MJADALA WA HITIMISHO LA MAFUNZO YA ISAVET CHUO KIKUU CHA SUA, MOROGORO

14 days ago
6

Siku hiyo ilikuwa ya jua kali huku upepo mwanana ukivuma kutoka milima ya Uluguru, ukichangia hewa safi na baridi pembezoni mwa ukumbi wa mikutano uliopo Chuo Kikuu cha Kilimo na Mifugo (SUA) mkoani Morogoro. Hapa ndipo mjadala muhimu uliohusu hitimisho la mafunzo ya In-Service Applied Veterinary Epidemiology Training-ISAVET yaliyoandaliwa na FAO Tanzania ulifanyika.

Washiriki walikusanyika kwenye moja ya kumbi ndogo za mikutano pembezoni mwa ukumbi mkuu wa mikutano, kujadili mafanikio na changamoto za programu hiyo.

Ufunguzi wa Mjadala:
Dr. Moses Ole Neselle kutoka FAO, akiwa ni msimamizi wa programu hiyo, alianza kwa shukrani za dhati kwa washiriki wote waliohudhuria na kwa mchango wao muhimu katika mafunzo hayo.

“Mafunzo ya ISAVET yamelenga kuboresha ufuatiliaji na usimamizi wa magonjwa ya mifugo. Leo tuko hapa kujadili tuliyojifunza na jinsi tunavyoweza kuboresha zaidi katika siku zijazo,” alisema Dr. Neselle kwa msisitizo.

Ushuhuda wa Washiriki:
Bi. Asha Zahran, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mifugo kutoka Zanzibar, alikuwa wa kwanza kutoa maoni yake. Alielezea jinsi mafunzo yalivyoboresha ufuatiliaji wa magonjwa huko Zanzibar. “Kupitia mafunzo haya, tumeweza kuboresha mfumo wetu wa taarifa za magonjwa na kuweka mikakati madhubuti ya kudhibiti magonjwa yanayotishia mifugo yetu,” alisema Bi. Asha kwa shauku.

Fusebia Mussa, mshiriki wa mafunzo kutoka Wilaya ya Tanganyika, alisimama na kutoa ushuhuda wake. “Kupitia haya mafunzo hakika nimeongeza ujuzi mkubwa na nitakapo rejea kituoni kwangu nitafanya mabadiliko makubwa hususani katika ufuatiliaji wa magonjwa ya mifugo, na ikiwa nipamoja na uchukuaji wa hatua za kuyadhibiti,” alielezea Fusebia akionyesha matumaini makubwa baada ya program hiyo.

Bi. Wantere Maswe kutoka Kituo cha Mifugo cha Ramadi wilayani Busega, alieleza jinsi mafunzo hayo yanavyoweza kumsaidia katika kuboresha ushirikiano kati ya wakulima na wataalamu wa mifugo. “Mafunzo haya yamenifundisha mbinu za kuwasiliana vizuri na wakulima, na sasa tutafanya kazi pamoja kwa karibu zaidi kuhakikisha mifugo yetu inabaki na afya njema,” alisema Bi. Wantere kwa tabasamu.

Mjadala ulipofikia mwisho, Dr. Neselle alitoa hitimisho lake, akiwapongeza washiriki kwa mchango wao mkubwa. “Tumepata mengi kutoka kwa kila mmoja wenu. Haya mafunzo yameonyesha umuhimu wa ushirikiano na ufuatiliaji thabiti.

Tunahitaji kuendelea kuboresha mifumo yetu na kushirikiana kwa karibu zaidi, hata hivyo ni muhimu tuendelee kujifunza na kubadilishana taarifa. Pia, tunahitaji kuhakikisha mafunzo haya yanakuwa endelevu na yanafikia maeneo mengi zaidi, hususan vijijini,” alisema Dr. Neselle.

Loading comments...